Kikosi cha Simba Queens kinatarajia kutupa karata yake ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi na wataanza kucheza na AS FAR na mashindano hayo yanaanza kesho kutwa Oktoba 30 nchini Morocco.
Simba wameishi kwenye mji huo kwa siku nne, tangu walipofika kwenye nchi hiyo ambapo walipata muda wa kufanya mazoezi na kujiandaa na mashindano hayo ambapo Simba watakuwa wanaiwakilisha kanda ya Cecafa.
Kocha wa timu hiyo Charles Alex Lukula Ayiekho raia wa Uganda amesema kuwa kila kitu kinakwenda sawa kwenye klabu yake, na anatarajia kuwa vijana wake watafanya kazi kubwa ya kuweza kuvuna ushindi wa kwanza kwenye mashindano hayo makubwa Afrika.
Simba Queens wamepangwa kundi A na klabu za AS FAR ya Morocco, Determine Girls ya Liberia na Green Buffaloes ya Zambia. Kundi B kuna timu za Mamelodi Sundowns, Bayelsa Queens FC ya Nigeria, Wadi Degla ya Misri na TP Mazembe ya Dr Congo.