Simba chini ya kocha mkuu wa muda, Juma Mgunda, ilikuwa imejipa mwiko kuwa haitapoteza mechi yoyote msimu huu kirahisi, lakini jana Azam FC wamevunja mwiko huo.
Katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba ilikumbana na kipigo cha bao 1-0 na kubaki nyuma kwa tofauti ya pointi tatu dhidi ya mabingwa watetezi Yanga wanaokamata nafasi ya kwanza.
Simba ilikuwa na majeruhi kibao kuelekea mchezo huo ambapo Sadio Kanoute hakuwepo pamoja na Mzamiru Yassin, Shomari Kapombe ambao kutokana na matatizo ya majeraha na kadi waliikosa mechi hiyo.
Bao pekee la Azam FC katika mchezo huo lilifungwa na Prince Dube dakika ya 34 akitumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Simba kuiadhibu Simba nzima.
Habib Kyombo atajilaumu mwenyewe kwa kukosa nafasi mbili za wazi dakika ya 13 na 44 katika mchezo huo.
Matokeo hayo yanaifanya Simba ibaki na pointi 14 katika nafasi ya tatu huku Mtibwa wakiwa juu yao wakiwa na alama 15 lakini wakiwa wamecheza michezo miwili zaidi.
Yanga ni vinara wa msimamo wakiwa na pointi 17 baada ya kucheza michezo saba huku Simba wakiwa na pointi 14 baada ya michezo hiyo saba.
Huu ni mchezo wa kwanza kocha Juma Mgunda anapoteza tangu alipoanza kuinoa Simba katika michuano yote zikiwemo mechi za kimataifa na zile za kirafiki.
Kwa matokeo hayo, Azam wanapanda hadi nafasi ya nne wakiwa cna pointi 14, sawa na Simba lakini Azam wakiwa wamecheza mchezo mmoja zaidi.
Azam FC hii inaongozwa na kocha Kally Ongala akisaidiana na Aggrey Morris ambao ni wakongwe wa Azam tangu wakiwa wachezaji na inaonekana wameirudisha timu hiyo katika mbio za ubingwa.