Adhabu ya wakala maarufu duniani ya kuzuiliwa kabisa kujihusisha na mambo ya usajili kwa kipindi cha miezi kadhaa kwa hakika ni changamoto kubwa sana kwa watu wake ambao wapo chini ya soko lake kwa wakati huu maana wakala huyo hatoweza kujishughulisha katika hilo kwa sasa kutokana na adhabu hiyo.
Wakala huyo raia wa Italia anawakilisha majina makubwa ya wachezaji katika klabu mbalimbali kubwa ikiwemo ndani ya Manchester United akisimamia biashara ya Paul Pogba. Hata ndoto ya Pogba kutimkia Madrid inaweza kuwa ngumu sana baada ya shirikisho la soka duniani kumfungia kabisa kujihusisha na mambo ya usajili kipindi hiki.
Awali alikutana na adhabu hiyo kwa kutokujihusisha na mambo ya usajili kwa kipindi cha miezi mitatu ndani ya Italia pekee na hilo lilikuwa nafuu kwa sababu ilikuwa haiathiri biashara zake za sehemu nyingine lakini kamati ya maadili ya FIFA imepandisha adhabu yake na kuwa kubwa zaidi na sasa inasimamiwa na shirikisho hilo la soka la duniani.
Carmine na Vincenzo Raiola walikutwa na vitendo vya ukosefu wa kinidhamu kitu ambacho ni kinyume kabisa na sera za kisoka na halikubaliki kabisa. Wote hawa wanajihusisha na masuala ya soka na adhabu zao zimekuwa tofauti kidogo ambapo Carmine Raiola atatumikia adhabu yake kwa miezi mitatu na Vincenzo Raiola kwa miezi miwili.
Sio Pogba pekee na safari yake ya kujiunga na Madrid bali pia kapteni wa klabu ya Ajax, Matthijs de Ligt atakuwa hatarini kuchelewa kupata uhamisho wake. Japo tayari wakala huyo aliweka kivuli kwa kuhitaji gharama za usajili ambapo naye atahitaji kiasi cha £13 milioni na Barcelona na Ajax hawakuwa tayari kabisa kuzilipa fedha hizo.
Pia, mlinzi wa kati raia wa Ugiriki, Kostas Manolas ambaye alikuwa anahusishwa na kujiunga na klabu za Manchester United au Arsenal bado kutakuwa na ugumu kwake kutokana na sakata hilo la wakala wao. Jambo hilo linaweza kuvuruga mipango ya wengi au kuchelewesha safari za wachezaji wengi.
Mbali na hao, wachezaji wengine walio chini ya mikono ya wakala huyo ni Gianluigi Donnarumma [AC Milan], Kenny Tete [Lyon], Marco Verratti [PSG], Blaise Matuidi [Juventus], Henrikh Mkhitaryan [Arsenal], Justin Kluivert [Roma], Moise Kean [Juventus], Mario Balotelli [Marseille]. Hawa ni baadhi ya nyota ambao wapo katika soko la hali ya juu chini ya wakala huyo nguli duniani.

