Corona Ilivyoathiri Michezo Duniani

Mwishoni mwa mwaka 2019 mwezi Desemba zilitolewa habari za kuenea kwa ugonjwa wa kuambukiza wa virusi vya Corona huko Uchina. Ugonjwa huo unaoenezwa kwa njia ya hewa ulileta taharuki kubwa kutokana na kuzuka kwa vifo vya watu na wengine kuathiriwa au kukumbwa na maradhi ya ugonjwa huo.

Ubaya ni kuwa umeenea ugonjwa huo na kusambaa katika mabara mbalimbali: Asia, Ulaya hadi Afrika. Inakadiriwa kuwa watu takribani 90,000 wameambukizwa na 3000 wamefariki, hizo ni takwimu zilizofanywa mpaka kufikia mwezi Machi 2020, waathirika na vifo vingi vimetokea huko huko Uchina ingawa sehemu nyingine pia madhara yameonekana.

Ugonjwa huo umeleta kizaizai au hali ya sintofahamu hadi katika sekta ya michezo. Tokyo Marathon ni mashindano makubwa ya riadha ambayo hufanyika huko Japan katika jiji la Tokyo. Hujumuisha wanariadha kutoka nchi zote duniani. Ila mashindano hayo yaliingia dosari kutokana na maambukizi ya virusi vya Corona. Kwani watu wengi wameahirisha kwenda kushiriki hivyo kujumuisha washiriki wachache tu, kikawaida ilitakiwa washiriki 35,000 ila wameshiriki 300 tu. Pia, kuna wale wanaojitolea kushiriki mbio hizo ambao kawaida huwa elfu kumi ila wamejitokeza 600 tu. Mashabiki walikuwa wachache mno na wengi wao wakiwa wamevaa vitambaa vya kuzuia hewa puani na mdomoni. Kiujumla Tokyo Marathon mwaka huu imekosa msisimko ila hakuna namna kwani uhai ni muhimu zaidi.

Kwa upande mwingine, mbio za magari yaendayo kasi maarufu kama langalanga zilizotakiwa kufanyika huko Uchina ziitwazo Chinese Grand Prix zimeahirishwa. Chinese Grand Prix zilizotakiwa zifanyike Aprili 19 zimeahirishwa hadi hali ya kiusalama ikiwa sawa. Shirikisho la mbio hizo FIA Fédération Internationale de Automobile limezungumza na lile la Uchina Federation of Automobile and Motorcycles Sport of Republic of China na kufikia uamuzi huo. Wameongea na timu zilizotakiwa kushiriki pamoja na mapromota hivyo kufikia uamuzi wa kuahirishwa hadi hali ya kiusalama itakapokuwa sawa.

Katika mchezo wa soka mambo pia yalikuwa si mazuri hususan kwenye ligi ya Italia. Kwani mechi kadhaa ziliahirishwa ikiwa mechi mbili za Copa Italia kati ya Juventus na AC Milan na ule wa Inter Milan na Napoli. Kutokana na wachezaji watatu wa Minnows Piannese kugundulika wana maambukizi ya virusi hivyo, Juventus chini ya miaka 23 ambao walipambana na timu hiyo katika ligi daraja la tatu au Seria C, Juventus wamelazimika kuvunja kambi za hao vijana ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.

Ila katika hali ya kuweka msisitizo zaidi ilipelekea michezo ya ligi kucheza pasi na mashabiki. Hebu tathmini ni namna gani michezo hiyo ilikosa radha ya uhamasishaji kutoka kwa wapenzi na mashabiki wa timu hizo.

Rais wa FIFA, Bwana Gianni Infantino amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kuziahirisha mechi za kimataifa ili kuepuka kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa huo. Infantino amenukuliwa akisema, “The health of the people is more important than any football games and anything!” akimaanisha kuwa afya za watu ni bora kuliko michezo na kila kitu hivyo ni muhimu kuangalia usalama wa watu kwanza. Ikumbukwe kuwa salamu za kupeana mikono nazo hazifai kwani nazo huchochea maambukizi, ajabu iliyoje maana kupeana mikono ni njia mojawapo ya kuonesha kuwa soka ni mchezo wa kiungwana.

Ngoma nzito hii jamani, tuendelee kuomba Mungu Atuepeshie mbali na hili balaa, Amin.

4 Komentara

    Mungu atuepushe na Hili janga
    La corona

    Jibu

    Colona umekuja kuharibu kila kitu

    Jibu

    Corona majanga kwl

    Jibu

    Ni mungu tu hatusaidie

    Jibu

Acha ujumbe