Wakati ligi nyingi zikiwa zimesimsmishwa kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na kirusi cha Corona (COVID 19), ni kipindi ambacho makocha wa timu mbalimbali wanakitumia kutathmini mapungufu ya vikosi vyao na namna wanavyoweza kufanya mabadiliko ili kuleta ushindani katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki. Hii ndiyo sababu tetesi za usajili zimekua nyingi kipindi hiki ambacho hata sio kipindi cha dilisha la usajili kwa ligi mbalimbali.
Sote tunakubaliana kuwa, hakuna timu ambayo huwa inakua na tetesi nyingi za usajili kama Man United. United ni kama huwa wanahusishwa na kila mchezaji mzuri aliyepo sokoni.
Tetesi zilianza kwa United kutaka kumsajili mshambuliani wa Tottenham Hotspur Harry Kane. Dili hilo lilichagizwa na dalili zilizooneshwa na Kane mwenyewe kuonesha kuwa anataka kuondoka Tottenham, anataka mafanikio katika soka na timu zilizoonesha nia thabiti ya kuhitaji huduma yake ni Real Madrid na Manchester United huku Kane mwenyewe akionesha kupendelea zaidi kwenda United. Mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy anaitumia fursa hiyo kutaja dau kubwa la paundi 200 milioni hali inayoleta ugumu wa dili hilo kukamilika. Kabla hilo la Harry Kane halijaisha kukaibuka jingine la Jadon Sancho.

Sancho ni winga hatari wa Borrusia Dortmund mwenye asili ya Uingereza. Kabla kinda huyo hajatua Dortmund kulikua na kila dalili angesajiliwa na United lakini dili hilo likakwama kutokana na United kuona kuwa Mino Raiola, wakala wa mchezaji huyo ameweka vipengele vingi katika mkataba wa mchezaji huyo na United ambavyo vinamfaidisha yeye zaidi, wakaachana nae. Huko bundesliga kinda huyo mwenye umri wa miaka 20 tu ameshakua gumzo, katika michezo 23 aliyocheza ameshafunga magoli 14 huku akiwa na pasi 16 za mabao. Sancho amekua Sancho kweli, united wanaanza kujisogeza tena.
Kuna kila dalili Sancho ambaye thamani yake inatajwa kuwa paundi 102m akatia saini united, baadhi ya vyanzo vya habari vinaripoti kuwa United wameshamalizana na Sancho mwenyewe bado tu kumalizana na Dortmund. Kabla hilo halijaisha likaibuka jingine la Jack Grealish.
Usajili wa kiungo huyo wa Aston Villa unaweza kuwa ndiyo usajili pekee wenye uwezekano mubwa wa kutimia miongoni mwa sajili zote zinazotajwa. Jack Grealish amekuwa na kiwango kizuri ndani ya kikosi cha Aston Villa licha ya ukweli kuwa timu yake haifanyi vizuri na inaelekea kushuka daraja, timu yake ni kama Imeshampa mkono wa kwa heri nahodha wao huyo hivyo kuipa Manchester United uwezekano mkubwa wa kuipata saini ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 ambaye thamani yake sokoni inatajwa kuwa paundi 80 milioni.
United pia wanatajwa kuhusishwa na nyota James Maddison anaekipiga kama kiungo mshambuliaji katika klabu ya Leicester City. United wapo katika harakati za kuimarisha safu yao ya ushambuliaji hivyo huduma ya kiungo huyu ambaye katika msimu huu amefanikiwa kucheza michezo 28 na kutupia kambani magoli 6 haikwepeki. Thamani ya Maddison sokoni ni paundi 60 milioni.

Huku hayo hayajakaa sawa kuna tetesi mpya tena kuwa United wanamfukuzia winga wa Shaktar Donetsk Kenny Tete.
Kuna sehemu nilipita nikasikia mashabiki wa United wanajadili kama je, wamsajili Neymar au Mbappe? Mmoja akasema kuwa ni bora wamchukue Mbappe kwani Neymar ni mtu mzima anaeishi katika utoto wake. Mwenzie akamjibu kuwa Neymar anafanya ule utoto ni kwakua hawahitaji PSG lakini hajawahi kufanya huo utoto akiwa Barcelona. Nilipita nikawaacha wakijadili huku nikitegemea labda baadae nitasikia au kuona katika vyombo mbalimbali vya habari kuwa Ole Gunnar Solskjaer amenukuliwa sehemu kuwa anamtaka mmoja kati ya Neymar au Mbape. Sikuwahi kusikia mpaka kesho, sijui walianzia wapi wale ndugu japo sijui pia walipoishia.
Suala la msingi la kujiuliza ni iwapo kweli mwalimu Ole Gunnar Solskjaer ana uhitaji wa wachezaji wote hao wanaotajwa au ni muendelezo tuu wa stori za kwenye vijiwe vya kahawa? Na hata kama ni kweli Solskjaer anahitaji huduma ya wachezaji hao, klabu ina msuli wa kutosha kuwasajili?
Ni wazi kuwa timu haiwezi kusajili kila mchezaji mzuri aliyepo sokoni. Na bahati mbaya katika kipindi hiki cha Corona sidhani kama kuna timu inaweza kufanya sajili mbili za gharama kubwa katika dirisha moja.
Mashabiki wa United lazima wajifunze kuacha kutaka ‘nyingi nasaba’ mana siku za hivi karibuni tuu wameletewa msiba, na msiba wenyewe ni kuwa Makamu Mwenyekiti Mtendaji wa United bwana Ed Woodward amesema (mashabiki) waache kufikiria vitu visivyowezekana. Woodward anasema kutokana na janga la Corona hategemei kutumia paundi 100+ milioni katika msimu huu. Tafsiri yake ni ipi? Ni wazi kuwa kwa bajeti hiyo United hawatoweza kumudu kusajili wachezaji hao yani Harry Kane, Sancho, Maddison, Grealish na wote wanaotajwa. Kilichobaki ni isajili mmoja au ikose wote, msiba kwa mashabiki wa United.


Furahav
Corona itaisha tu.
Issa
United ni timu kubwa ina uwezo pia
Johnmary joel
Waongeze bidii#meridianbett
farida ahmadi
Man United ni klabu kubwa Sana hinaweza kumsajili mchezaji yeyote yule na inabidi wakaze buti United kutokana na kupoteza gemu nyingi Sana hivyo hata kane akienda United inabidi wote wawe na ushirikiano wachezaji wote