Winga wa klabu ya Manchester United Jadon Sancho ameripotiwa kurejea rasmi kwenye mazoezi ya klabu hiyo baada ya kukosekana kwa kipindi kirefu.
Jadon Sancho hajafanya mazoezi na timu ya kwanza ya Manchester United tangu mwezi wa kumi na moja mwaka jana kutokana na matatizo binafsi ambayo yalikua yanamkabili mchezaji huyo. Lakini taarifa zinaeleza mchezaji huyo amerudi kufanya mazoezi na timu ya kwanza.
Mchezaji huyo iliarifiwa alikua anafanya mazoezi binafsi nchini Uholanzi ikiwa ni ushauri wa kocha wa klabu hiyo Erik Ten Hag, Siku chache ziilizopita mchezaji huyo alionekana katika dimba la Old Trafford ikiwa na maana amemaliza programu ya mazoezi binafsi aliyokua akiifanya nchini Uholanzi.
Jadon Sancho amekua akipitia kipindi kigumu ndani ya klabu ya Manchester United tangu kujiunga klabuni hapo mwaka 2021 kutokana na kucheza chini ya kiwango, Sababu iliyomfanya kupatiwa programu maalumu itakayomrudisha kwenye ubora wake.
Inatarajiwa mchezaji Jadon Sancho kuwepo kwenye sehemu ya kikosi cha Manchester United kitakochosafiri kuelekea jijini London katika mchezo wa ligi kuu ya Uingereza dhidi ya Crystal Palace utakaopigwa katika dimba la Selhurst Park siku ya Jumatano.

