Kama kusafiri na kufanya utalii ni kitu unachokipenda basi bado hujasafiri vya kutosha ikiwa hujawahi kutembelea kisiwa cha Madagascar, kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani kikitanguliwa na visiwa vya Greenland, New Guinea na Borneo.
Yapo mengi ya kufanya ndani ya Madagascar. Ukiwa katika mbuga ya taifa ya Isalo utaona wanyama wengi ikiwemo makundi ya nyani aina ya Lemurs wasiopatikana sehemu yoyote ile duniani, nenda Nosy Be ukaone mandhari ya kuvutia ya kisiwa hicho. Kama bado hujachoka unaweza kutoka kilomita 50 tu kutoka mji mkuu kisiwa hicho Antananarivo kutazama mlima wa kuvutia wa Ankaratra wenye asili ya volkano huku njiani ukifurahia virudi nyuma kama miti mikubwa aina ya Baobabs yenye umri wa miaka zaidi ya 800 iliyopo pande zote mbili za barabara kuelekea huko.
Jioni ukirudi Antananarivo kama wewe ni mtu wa ‘totozi’ unaweza kujisogeza mitaa ya Antsiranana pale kuna bonge moja la klabu ya usiku wenyeji wanapaita Le Taxi Be. Pale utapata fursa ya kufurahia muziki, pombe na wasichana wazuri wa kimerina, Betsileo na wageni.
Kama wewe starehe yako ni mpira kama mimi basi hapo Taxi Be hapakufai, chukua taxi mwambie dereva akupeleke Mojo by No Comment. Hapa zaidi ya pombe na wasichana wazuri utapata fursa ya kutazama matangazo ya moja kwa moja ya mechi za mpira wa miguu. Mijadala mingi hufanyika hapa hasa ikizingatiwa kuwa ni sehemu ambayo inakusanya wapenda soka wengi wa mji huu wa Antananarivo.
Mjadala wa nini kilifanyika hadi kufanya timu ya taifa ya Madagascar kufanya vizuri katika mashindano ya AFCON kati yangu na rafiki zangu ulianzia hapa Mojo by No Comment tukiangalia mechi ya robo fainali kati ya Madagascar dhidi ya Tunisia ambapo licha ya kupoteza kwa mabao matatu bila lakini kiwango walichokionesha hakikua haba. Ile kushiriki mashindano kwa mara ya kwanza na kufika hatua ya robo fainali ni zaidi ya ndoto kuwa kweli. Mimi na marafiki zangu hatukufikia muafaka usiku ule, nilijipa homework kulifuatilia hilo. Tukala kilaji usiku ule ukapita.
Sasa na hili janga la CORONA nimekua sina la kufanya, nimeangalia marudio ya mechi mpaka nimechoka. Nimesikiliza tetesi za usajili hadi nimeanza kuchanganyikiwa, naona rangi tu. Ghafla nikakumbuka kuifanya ile homework niliyojipa usiku ule wa Alhamisi ya July 11 2019 pale Mojo by No Comment.
Uchunguzi wangu ukanikumbusha kitu kimoja cha kushtusha zaidi kuwa Madagascar hawakufuzu Afcon ki bahati bahati. Japo ilikua mara ya kwanza kwa taifa hilo kushiriki mashindano hayo tangu yalipoanzishwa mwaka 1957, walifuzu kwa kupita katika kundi gumu lililokua na timu za Senegali, Equatorial Guinea na Sudan. Madagascar walifuzu kwa kuongoza kundi wakijikusanyia alama 10 yani juu ya Senegal ambao walikua na alama 7 tu!
Ikumbukwe pia kuwa Madagascar walipenya mpaka hatua ya robo fainali baada ya kuzifunga timu ngumu za Nigeria, Burundi na Congo. Waliwezaje?
Madagascar wakiwa taifa maskini kama ilivyo Tanzania tu hawakufika pale kama bahati. Waliweka mipango na mikakati kama taifa ili kufikia pale walipotaka.
Madagascar waliichagua nchi ya Hispania kama kesi yao ya kujifunzia. Zipo sababu ni kwanini waliichagua Hispania, waliangalia mafanikio yaliyofikiwa na Hispania katika soka kuanzia ngazi ya vilabu mpaka timu ya taifa. Lipo la kujifunza hapa, hujiulizi kwa nini hawakutaka kujifunza kwa nchi kama Pakistan, India au nchi zingine kama hizo ambazo hazina mafanikio yoyote katika soka? Tunashauriwa kujifunza kwa waliofanikiwa, waliofeli hawaishiwi maneno na sababu za kwa nini hawajafanikiwa. Uchaguzi wa Hispania kama sehemu ya kujifunzia ni wa kupongezwa.
Iliwachukua Madagascar miaka mingi kuusoma na kuuelewa mfumo wa soka wa Hispania. Waliichukua Hispania Ulaya wakaitua Antananarivo kama ilivyo. Wakajifunza namna Hispania wanagundua na kuendeleza vipaji vya soka kwa wachezaji tangu wakiwa wadogo kabisa. Wakajifunza sera za uendeshaji wa mpira kuanzia ligi ya ndani, shirikisho la soka na vilabu vya ligi yao kuanzia daraja la kwanza mpaka ligi kuu.
Haikua safari rahisi kwa Madagascar, iliwahitaji subira na kujitoa kweli kweli.
Wakati wengi wakifikiri kuwa Madagascar walifika robo fainali ya AFCON kama bahati au muujiza, ukweli ni kwamba yale yalikua matunda ya juhudi na uwekezaji mkubwa walioufanya kwa miaka mingi.
Madagascar kuileta Hispania Afrika wamefanya kama Serikali ya Zimbabwe chini ya uongozi wa Hayati mzee Mugabe ilivyofanya mwaka 2017 kuileta Brazil Afrika kwa kuchagua wanawake 10 na kuwapeleka Brazil ili wakapewe ujauzito na magwiji wa soka nchini humo lengo likiwa ni kuleta vipaji katika soka la Zimbabwe kama Brazil, Zimbabwe nao waliishusha Brazil Afrika kwa namna yao.
Acha kushangaa hutomaliza, muhimu tuchague tunajifunza kwa nani kati ya Madagascar au Zimbabwe.


Neema juma
Habari njema sana
Povel
Habar njema