Pale mwanzo United walitakiwa kulipa hela ya kihistoria itakayovunja rekodi nyingi zilizowekwa kama bado wangehitaji kumnasa mlinzi wa timu ya taifa ya Uingereza, Harry Maguire. Hilo lilikuja pale ambapo mchezaji huyo alizidi kupanda thamani ndani ya kikosi hicho kwa klabu ya Leicester kuweka dau lao la juu ambalo ni £90m kwa yeyote mwenye mapenzi ya kumhitaji nyota huyo.
Mashetani Wekundu walimhitaji mchezaji huyo hata kabla ya msimu huu na walifikia gharama ya £75m kwa kutaka kukamilisha kabisa usajili wake lakini jambo hilo liligonga mwamba kutokana na klabu inayommiliki mchezaji huyo kusimamia suala la gharama wanayohitaji kumuachia nyota huyo.
Huku kukiwa na ugumu wakati ule na ubovu wa safu ya ushambuliaji, walihitaji mtu ambaye ataweza kukipa nguvu kikosi hicho hasa eneo lao lenye majanga makubwa sana katika kampeni za ubingwa na kuweka mambo sawa wakaamua kurudi kumuwinda kwa awamu nyingine lakini ughali wa mchezaji huyo ukaibuka na kuwa wa juu sana.
Baada ya kusajiliwa kutoka Hull mwaka 2017 mlinzi huyo aliweza kuongeza upekee zaidi ndani ya kikosi hicho kwa kuweza kukipa matokeo hadi kukisimamia kiweze kuleta ushindani kwa klabu yoyote wanayokutana nayo. Pia, aliweza kukiongoza kikosi cha timu ya taifa kwenye michuano ya Euro iliyopita na pia kwenye kombe la dunia.
Katika miaka yake 26 kiwango chake kikaendelea kupanda kwa kasi kutokana na uwepo wa wachezaji. Na endapo angefanikiwa kutua basi katika makazi yake mapya ni hakika angechagiza sana kuifikisha timu hiyo mbali zaidi katika ramani za kimataifa na kwenye mashindano mengine yote ya ndani.
Kwa wakati ule walichohitaji ni nani wa kusaidiana na Lindelof katika harakati hizo. Kwa sababu tangu mchezaji huyo asajiliwe 2017 alijaribu kuonesha kitu fulani cha pekee kikosini hapo kilichofanya angalau mapungufu yaliyooneshwa mara kwa mara na wachezaji anaofanya nao kazi uwanjani.
Endapo biashara ile isingepewa nafasi kama matarajio ya klabu hiyo yanavyoonesha basi matajiri hao wangerudi nyuma kumuwinda kwa mara nyingine Koulibaly ambaye wamemuweka kipaumbele katika mipango yao kwa kipindi kirefu. Mchezaji huyo amekuwa na mchango mkubwa sana ndani ya Napoli na hilo linawapa nguvu United.
Ni imani ya kila mmoja kwamba mchezaji mara nyingi hutamani sana kucheza kwenye klabu ambayo inaonesha kutwaa sana mataji na ina malengo makubwa ya muda mrefu. Kwa nafasi hiyo Leicester hawakuwa na nafasi kubwa kuendelea kumshawishi sana Maguire abakie viwanja hivyo. Na kama angeamua kutimka hawangeweza kumzuia kabisa.

