Ballon d’Or ni kati ya tuzo zenye heshima sana kwa mchezaji na hiyo ni tuzo anayokabidhiwa mchezaji ikiwa haihusiani kabisa na ngazi ya klabu yake. Miongoni mwa wachezaji wakubwa kabisa duniani hupiganiana sana kila msimu ili kuinyanyua tuzo hiyo ya heshima sana.
Luka Modric aliinyanyua tuzo hiyo mwaka jana baada ya kuwa na msimu mzuri sana aliouonesha akiwa na klabu ya Real Madrid pia timu yake ya taifa kwenye michuano ya kombe la dunia na kufanikiwa kuvunja rekodi za watawala wawili wa tuzo hiyo ambao ni Messi na Ronaldo.
Pamoja na Modric kuvunja mapokezano hayo ya wachezaji hao wawili kwenye tuzo hiyo lakini ni vigumu sana kuizungumzia tuzo hiyo bila kuwataja wawili hao. Messi na Ronaldo wametawala tuzo hiyo wakibadilishana kwa miaka mingi huku wakionesha upinzani wa aina yake na soka la kipekee sana.
Messi (31) ameendelea kuonesha ubora wake zaidi ndani ya kikosi cha Barcelona akiwa anafunga magoli wakati wowote ule akipata nafasi ndani ya timu hiyo hata kwa kulazimisha ushindi wakati wakiwa kwenye hali isisyo ya kawaida. Na hata sasa anashukuriwa kwa kuwafikisha Wakatalunya kwenye fainali ya Copa del Rey.
Raia huyo wa Argentina anafukuzia kiatu cha ufungaji Ulaya akiwa na magoli 34 msimu huu, pia anaongoza kwa wingi wa magoli ndani ya michuano ya klabu bingwa Ulaya mbali na klabu yake kutupwa nje. Mbali na hilo kuna vitu vina uwezekano mkubwa kumzuia Messi kutwaa tuzo hiyo mwaka huu kama vile:
Kutupwa nje kwenye michuano ya klabu bingwa, tumeshuhudia vichapo vikubwa ambavyo klabu nyingi zimekutana navyo ndani ya michuano hiyo. Na kikubwa zaidi ni kile cha Barcelona kupigwa 4-0 Liverpool. Na kwa miaka mingi tumeona kwamba mafanikio ya ndani pekee hayampatii mchezaji tuzo hiyo hivyo Messi anaweza kuikosa pia kwa hilo.
Kuibuka kwa washindani wakubwa zaidi, uwepo wa wapinzani kama Virgil van Dijk kwa hakika ni kikwazo kwa Messi kunyanyua haraka tu tuzo hiyo. Wamekuwa na mchango mkubwa maradufu zaidi ya Messi msimu huu. Pia, watu kama Kylian Mbappe na Mohamed Salah hawawezi kupuuzwa kwa takwimu zao za msimu huu.
Hivi vinaweza kuwa vigingi kwake kunyakua tuzo hiyo ya heshima, pia, mbali na hilo ana kigingi kingine ndani ya taifa lake akiweza kutupwa nje kwenye michuano ya Copa America jambo ambalo linamyima tena alama zaidi baada ya kupigwa na Venezuela.

