Timu ya taifa ya Uholanzi chini ya kocha louis Van Gaal imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuibamiza timu ya taifa ya Marekani kwenye hatua ya 16 bora mapema leo.
Vijana wa Louis Van Gaal wamefanikiwa kuichakaza timu ya taifa ya Marekani kwa jumla ya mabao matatu kwa moja katika mchezo uliopigwa katika dimba la Khalifa International na kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali.
Mabao ya Mephis Depay, Daley Blind, pamoja na Denzel Dumfries yalitosha kuwapa Uholanzi ushindi huku bao la kufutia machozi la timu ya taifa ya Marekani likifungwa na Haji Wright na kutupwa nje ya michuano hiyo.
Timu ya taifa ya Uholanzi wanasubiri mshindi wa mchezo wa usiku kati ya timu ya taifa ya Argentina dhidi ya Australia ambapo atakaeshinda hapo anaelekea kumenyana na Uholanzi ambaye tayari ameshafuzu jioni ya leo.
Kama itatokea hatua ya Robo fainali watakutana Uholanzi na Argentina basi itakua ni mechi ya kisasi baina ya wababe hao, Kwani Uholanzi watahitaji kulipiza kisasi pale walipotolewa kwenye hatua ya nusu fainali mwaka 2014 Brazil kwenye michuano ya kombe la dunia.

