YANGA WATOA TAARIFA RASMI KUHUSU NABI

HATIMAYE UONGOZI wa Yanga umetoa taarifa rasmi juu ya kile kilichodaiwa kuwa umefukuza kocha wake mkuu Nasreddin Nabi na msaidizi wake Cedric Kaze kwa kushindwa kuvuka na kwenda hatua ya makundi ligi ya mabingwa.

Taarifa hiyo ilisema: “Tunapenda kuwataarifu mashabiki na Wanachama wake kuwa Nasreddin Nabi, bado ni kocha mkuu wa timu yetu.

“Nabi alijiunga na Yanga April, 2021 na amekuwa na rekodi nzuri ya kuiongoza timu yetu kubeba Ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, bila kupoteza.”

Akizungumza na YANGA MEDIA, Mtendaji Mkuu wa Yanga, Andre Mtine amewaomba mashabiki na wanachama wa Yanga kufatilia taarifa za uhakika za timu yao kupitia vyanzo rasmi vya habari vya klabu.

“Niwaombe mashabiki na wanachama wetu kuwa na utaratibu wa kufatilia taarifa za klabu yetu kutoka kwenye vyanzo vyetu vya habari.

“Tuna YANGA APP. Tuna Website ya Young Africans na kurasa zetu za mitandao ya kijamii ambazo zimekuwa zikitoa taarifa za klabu yetu na kwa wakati sahihi,” alisema Andre.

Uongozi unamtakia kila la kheri kocha Nabi na benchi lake la ufundi kwenye maandalizi ya mchezo wa kesho wa Ligi Kuu dhidi ya KMC utakaopigwa saa 1:00 jioni kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa.

Acha ujumbe