KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Farid Mussa, ameondolewa katika kambi ya timu hiyo, kutokana na maumivu ya misuli aliyoyapata mazoezini.
Nyota huyo aliondolewa katika msafara wa timu hiyo, uliosafiri kwenda Mbeya kucheza dhidi ya Ihefu jana Jumatano, kisha Jumamosi hii wakiwa na mchezo Mwanza, dhidi ya Geita Gold.Taarifa ambazo zinasema kiungo huyo aliondolewa kabla ya safari ya Mbeya ambapo amebaki Dar ili kuhakikisha anapona na kurejea kuipambania timu hiyo.
Aliongeza kuwa, upo uwezekano mkubwa wa kiungo huyo kurejea uwanjani mapema, kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi hicho katika michezo ijayo.
“Farid Mussa tumembakisha Dar es Salaam kwa ajili kuendelea matibabu, baada ya kupata majeraha tukiwa mazoezini tukijiandaa na mchezo dhidi ya Ihefu.
“Mara baada ya majeraha hayo, alifanyiwa vipimo na kuonekana majeraha yake makubwa, hivyo ataukosa mchezo huu dhidi ya Ihefu.“Lakini atajiunga na timu kambini, mara baada ya timu kurejea Jijini Dar es Salaam baada ya mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Muargentina, Miguel Gamondi, alisema: “Kikosi chetu kipo tayari na fiti kupambana dhidi ya Ihefu, lakini nitawakosa baadhi ya wachezaji wachache kutokana na majeraha akiwemo Farid Mussa.”