Klabu ya soka ya Yanga imeanza vibaya katika michuano ya kombe la shirikisho Afrika baada ya kukubali kichapo cha mabao mawili kwa bila dhidi ya klabu ya US Monastir ya nchini Tunisia.
Klabu ya Yanga wakiwa ugenini wamekubali kupokea kichapo cha mabao mawili kwa bila mapema kabisa kipindi cha kwanza mabao ambayo yamedumu mpaka mwisho wa mchezo na kuwafanya wananchi kupoteza mchezo wao wa kwanza wa makundi msimu huu.
Mabao ya US Monastir yalifungwa Saghraoui dakika ya 10 ya mchezo na Traore akifunga bao la pili dakika ya 16 ya mchezo huo na kuwafanya miamba hiyo ya soka nchini Tunisia kuibuka na alama tatu katika mchezo huo, Hivo kuwafanya kuanza vizuri mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi ya kombe la shirikisho Afrika.
Zikiwa zimepita takribani siku 94 tangu klabu ya Yanga wapate matokeo mazuri katika ardhi ya Tunisia baada ya kuifunga klabu ya Club Africain kwa bao moja kwa bila na kuweza kufuzu hatua ya makundi Afrika, Lakini leo haikua hivo kwani Wananchi walikubali kichapo cha mabao mawili kwa bila katika mchezo huo.
Klabu ya Yanga sasa wana mtihani katika mchezo wao wa pili wa makundi kombe la shirikisho Afrika kwani watakua na kazi ya kuikaribisha klabu ya Tp Mazembe katika mchezo utakaopigwa Jumapili ijayo katika dimba la Benjamin Mkapa,Wananchi watahitaji kupata matokeo katika mchezo ili kuendelea kuweka matumaini ya kuweza kufuzu hatua ya robo fainali ya kombe la shirikisho msimu huu.

