800m za Chama, Utani wa Jadi Au Dhihaka kwa Yanga?

Utani maana yake ni maneno au matendo yenye kejeli au masihara kwa lengo la kuchekesha. Utani huzingatia mrejesho wa hisia kutoka kwa mtu anayefanyiwa utani, yaani usilete madhara upande wa pili iwe ya kimwili au kihisia.

Kwa upande mwingine, dhihaka ni maneno au matendo yanayoambatana na masihara, ni aina ya kejeli yenye ubeuzi mkali ambao humuumiza mtu kihisia. Suala la utani wa jadi baina ya timu za Simba na Yanga lipo kwa makumi ya miaka sasa. Tangu kipindi hicho Simba ikiitwa Sunderland, The Queens na hatimaye Simba. Kuna sababu nyingi za kuwepo kwa utani huo, ukiacha uhasimu wa uwanjani zipo pia sababu zinazotokana na tofauti za kijamii, kisiasa na mtindo wa maisha.

Hili la historia ya ‘…utani wa jadi’ tutaliangalia siku zijazo panapo majaaliwa, leo tuliangazie hili la Cloutus Chama ‘Mwamba wa Lusaka’ na Yanga. Kama wewe ni mpenzi wa soka utakua hujapitwa na tetesi za hivi karibuni juu ya klabu ya Yanga kupitia kwa makamu mwenyekiti wake, Fedrick Mwakalebela kukiri kuhitaji huduma ya mchezaji wa Simba, Cloutus Chama almaarufu ‘Mwamba wa Lusaka’. Mwakalebela alienda mbali zaidi na kudai kuwa tayari klabu yake imeshafanya mazungumzo na mchezaji huyo na siku si nyingi atatia saini kuwachezea Wanajangwani.

Joto lilipanda haswa katika suala hilo hadi kufikia hatua ya klabu ya Simba kupitia CEO wake Bwana Senzo kuwasilisha barua ya malalamiko TFF wakilitaka shirikisho hili liichukulie hatua klabu ya Yanga kwa kosa la kukiuka kanuni za usajili. Ukiacha mengi yaliyosemwa na kutokea katika sakata hilo, kuna jambo muhimu wadau wa soka wanalisahau au kulipuuza, nalo ni kauli ya afisa habari wa Wekundu wa Msimbazi, Haji Sunday Manara akiwajibu klabu ya Yanga kuwa hakuna timu Tanzania yenye uwezo, acha tu wa kumlipa mshahara lakini pia kumsajili nyota huyo wa Chipolopolo. Haji Manara alienda mbali zaidi na kusema kuwa timu yoyote inayohitaji huduma ya mchezaji huyo iwe tayari kutoa kiasi cha pesa za kitanzania milioni 850! Maajabu haya.

Hivi huu ni muendelezo wa ule ‘UTANI wa jadi’ wa Simba na Yanga, au ni DHIHAKA kuwa Yanga hawana hicho kiasi cha fedha? Ni kweli kuwa kuna mchezaji yeyote Simba, Yanga au timu yeyote Tanzania mwenye thamani hiyo? Haji Manara anataka kutuaminisha kuwa ligi yetu imekuwa kiasi cha kuweza kuzalisha mchezaji mwenye thamani inayokaribia bilioni moja za kitanzania?

Ngoja kwanza, Manara anamzungumzia Chama huyu huyu ambaye hivi punde tuu Juni 18, 2021 anatimiza miaka 30? Umri wa jioni kabisa! Sote tunajua kuwa Chama huyu siyo Chama yule ambaye aliisaidia ZESCO United F.C. kufika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa ya CAF kabla ya kusaini mkataba na Al Ittihad ya Misri. Hata kipindi hicho Chama (kwa mujibu wa mtandao wa Transfermarket) alikuwa na thamani ya milioni 250 tu za Kitanzania.

Hivi sasa mambo mengi yamebadilika, Chama hafungi wala kusababisha pasi za mabao kama alivyokuwa akifanya akiwa Al Ittihad achia mbali akiwa Zesco. Chama thamani yake iliporomoka alivyosajiliwa Simba, huniamini mimi tembelea ukurasa wake katika mtandao wa Transfermarket kisha majibu kaa nayo.

Najua utagundua ni kwa namna gani ndugu Manara aliamua kwa makusudi kabisa kutuchekesha wadau wa soka, kwa upande mwingine kuwafurahisha wanazi na mashabiki wa Simba. Huku kwa kujua ama kutokujua akiwadhihaki Yanga.

2 Komentara

    Habar njema

    Jibu

    Gud news

    Jibu

Acha ujumbe

Meridianbet
Privacy Overview

This website uses cookies so that we can provide you with the best user experience possible. Cookie information is stored in your browser and performs functions such as recognising you when you return to our website and helping our team to understand which sections of the website you find most interesting and useful.