OFISA Habari wa Klabu ya Ruvu Shooting Masau Bwire amesema kuwa, mashabiki wa Simba na Yanga waache ushamba wa kujipendekeza kwa wageni kwenye kipindi hiki ambacho timu zao zinashiriki mashindano ya kimataifa.
Bwire, aliwataka mashabiki na wanachama wa Simba na Yanga kuacha kuwasapoti na kuwapokea wageni pindi wanapokuja nchini kucheza moja na timu hizo, badala yake washikane mkono ili kuvuka hapa na kwenda mbali zaidi.

Akizungumza kwa hisia kali Masau Bwire aliweka bayana: “Kumekuwa na tabia ambayo imezoeleka kwa miaka mingi sana kwa mashabiki wa Simba na Yanga kuwapokea wageni wanapokuja kucheza mechi za kimataifa hapa nchini.
“Kwangu naiita hiyo ni tabia ya kishamba ambayo inatakiwa kukemewa. Tunahitaji timu zetu zote ziweze kuvuka hapa na kwenda mbali. Hili kuvuka inatakiwa Watanzania wote tushikamane na kuwa kitu kimoja.
“Hii tabia ya kuwakarimu na kuwahudumia wageni haina faida hata kidogo. Niwaombe huu ni muda wa kuweka kando rangi za timu zetu na tusimame kama taifa.”
Simba, Yanga na Azam ndiyo klabu zilizosalia katika mashindano ya kimataifa baada ya Geita Gold FC kutolewa.

