OFISA Habari mpya wa Yanga Ali Kamwe amesema kuwa hajaenda kwenye klabu hiyo kumtumikia rais wa klabu hiyo Eng. Hersi Said bali amekwenda kuwatumikia mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga.

Ali Kamwe alisema, yeye kazi yake kubwa itakuwa ni kuisemea Yanga kwenye nyanja zote na kuchukua maoni ya wanachama na mashabiki wa Yanga yenye lengo ya kuijenga timu hiyo kwa uongozi wa juu ili kuweza kuyafanyia kazi.

Ali Kamwe alisema anajua nini anatakiwa kufanya ili kukata kiu ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo: “Mimi sijaenda Yanga ili kumtumikia Eng Hersi pekee yake, bali nipo hapa kwa ajili ya kuwatumikia wanayanga.

“Mimi ni kisemeo na mtumwa wa mashabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga, nitakuwa nawawakilisha kwenye kila eneo ambao nitakuwepo, kuwapa maendeleo ya klabu na maoni ya rais wetu kwenye kipindi hiki ambacho klabu inataka kuvunja miiko yote.

“Ndiyo maana nimesema, inatakiwa kwanza, mashabiki wote wa Yanga kuonyesha kuwa wapo tayari kunituma  kwa kuja kwa wingi uwanjani Oktoba 8 wakati tukicheza na Al Hilal.

“Huo utakuwa ujumbe tosha watakaonipa mimi na Kwenda kwa wachezaji na viongozi kwamba hawa watu wanahitaji furaha ili waendelee kujaa viwanjani.”

Kamwe alitangazwa juzi kuwa ofisa habari wa timu hiyo akichukua nafasi ya Haji Manara ambaye anatumikia kifungo cha miaka miwili chakuwa nje ya mpira.

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa