KAMA unafikiri kipigo cha mabao 2-1 walichofungwa Ruvu Shooting kimemuumiza sana kocha wa timu hiyo Boniface  Mkwasa basi ni tofauti kwani yeye anaona timu yake imecheza vizuri na kubwa zaidi kumzuia straika hatari wa timu hiyo Fiston Mayele hakuweza kufunga.

Mkwasa alisema mchezo huo haukuwa rahisi kwao, kwani wachezaji wake walipambana kufa na kupona kwa dakika zote 90, na hata kufungwa kwao kulitokana na makosa madogomadogo ambayo ni kawaida kutokea kwenye mechi.

Mkwasa alisema mabeki wake walifanya kazi kubwa mno na kwake anaona Faraja kwa kuwa Mayele hakufurukuta na hakuweza kufunga bao kwenye mchezo huo, ambao wafungaji walikuwa ni Feisal Salumu na Bakari Mwamnyeto.

“Vijana walijitahidi kuwa makini na walifanya kazi nzuri ya kuzuia na hata wale ambao huwa wanatetema hawakutetema. Kwahiyo mechi ilikuwa nzuri na tunajipanga kwa mechi inayofuata.

“Kilichotokea hadi kupoteza mchezo ilikuwa ni mistake za kawaida sana kwenye mchezo wa mpira wa miguu. Hatuna budi kupambana kwenye mechi zijazo kuweza kusaka alama tatu muhimu,” alisema Mkwasa.

Yanga waliweka rekodi ya kucheza mchezo wao wa 42 pasipo kupoteza mechi hata moja, kwenye ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Ruvu Shooting uliochezwa juzi Jumatatu kwenye uwanja wa Mkapa.

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa