KUELEKEA mchezo wao wa Jumamosi dhidi ya Yanga, uongozi wa Simba umetamba kuwa kwao mchezo huo una maana moja kubwa, ambayo ni kuanza rasmi safari ya kurejesha makombe yao yote matatu ambayo waliyapoteza kwa mtani wao Yanga msimu uliopita.
Keshokutwa Jumamosi Simba wanatarajiwa kuwa wageni wa Yanga katika mchezo wa ufunguzi wa pazia la Ligi Kuu Bara watakapovaana na Yanga, mchezo ambao unatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Yanga wataingia katika mchezo huo wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuifunga Simba bao 1-0, katika mchezo wa Ngao ya Jamii msimu uliopita wa 2021/22.
Simba msimu uliopita walipoteza mataji matatu kwa Yanga ambayo ni Kombe la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports na taji la Ngao ya Jamii, mataji ambayo walifanikiwa kushinda kwa misimu miwili mfululizo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Tunafahamu mchezo dhidi ya Yanga ni mgumu kutokana na historia ambayo imekuwepo kwa timu hizi mbili, lakini tuna lengo moja tu kuhakikisha tunarudisha makombe yetu yote ambayo tumeyapoteza msimu uliopita.
“Katika kufanikisha hilo ni lazima tuhakikishe tunashinda dhidi ya Yanga siku Jumamosi na wamekwisha kwa kuwa kikosi kipo tayari na kila mtu anajua tunachohitaji.”

