CAF: African Super League Kupigwa Mwakani

Historia mpya ya soka Afrika imeandikwa jana kwenye ardhi ya Tanzania jijini Arusha, kufuatia kutangazwa rasmi kwa mashindano ya maalum ya African Super League ambayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwezi Agosti, mwaka 2023 huku vigogo wa Tanzania Simba na Yanga wakiwa kwenye mtego mkubwa wa ushiriki wao.

Taarifa ya Shirikisho la soka Afrika (CAF), ambao ndio waratibu wa mashindano hayo, inaeleza kuwa yanaanzishwa kwa lengo la kutengeneza na kukuza thamani ya mchezo wa soka kupitia uwekezaji na wadhamini kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya soka Afrika.

Jumla ya zawadi za mshindano hayo zina thamani ya dola Milioni 100, ambazo ni sawa na zaidi ya Shilingi Bilioni 233 za Tanzania, huku mshindi akivuna dola Milioni 11.6 sawa na zaidi ya Shilingi bilioni 26.8 za kitanzania.

Shirikisho mwanachama wa mashindano hayo watavuna dola Milioni 1 sawa na Shilingi Bilioni 2.3 kwa mwaka, huku zaidi ya Bilioni 116.6 zikitengwa kwa ajili ya kusapoti soka la vijana na wanawake.

Mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha timu 24 kutoka mataifa 16 ya bara la Afrika, ambapo washiriki watatoka kwenye kanda tatu na kila kanda itatoa timu nane.

Timu saba kati ya hizo zitachaguliwa kulingana na mafanikio yao katika orodha ya ubora wa CAF kwa miaka mitano, huku timu moja ikipata nafasi kutokana na ukubwa wa soko la mashabiki wake na uthabiti wa uwekezaji walionao.

Ligi hiyo inatarajiwa kuanza rasmi mwezi Agosti mwaka 2023 na kukamilika mwezi Mei. Ligi hiyo itakuwa na jumla ya michezo 197 ambapo kwa timu moja itacheza michezo 21 mpaka kufanikiwa kufika fainali.

Acha ujumbe