Kikosi cha KMC kinachonolewa na Kocha Mkuu, Thierry Hitimana kimeanza mazoezi leo kujiandaa na mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold.
Mchezo huo unatarajiwa kupigwa Novemba 11 mwaka huu kwenye Uwanja wa Nyamkumbu, Geita.

KMC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Akizungumzia maandalizi yao, Ofisa Habari wa KMC, Christina Mwagala amesema “Baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Kagera Sugar wachezaji walipewa mapumziko na leo jioni wanaanza mazoezi.
“Matokeo yaliyopita hayakuwa rafiki kwa upande wetu lakini kwa sasa tunarejea tena mazoezini kwa ajili ya kurekebisha yale makosa yaliyojitokeza ili tupate matokeo mazuri.
“Timu yetu itaendelea kuweka kambi hapa Jijini Mwanza mpaka tutakapoenda kucheza mechi yetu ya pili ugenini dhidi ya Geita Gold.”

