BAADA ya kuanza kazi rasmi siku ya Jumapili, kocha msaidizi mpya wa Simba, Sbai Karim ameanza na mkwara mzito ndani ya kikosi hicho baada ya kutambulisha programu nzito ya mazoezi ya viungo na utimamu wa mwili kwa wachezaji wa timu hiyo, ili kuhakikishya wanakuwa fiti kuelekea msimu ujao hususani mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Simba wanaendelea na kambi yao ya kabla ya msimu nchini Misri ambapo kabla ya kuwasili kwa kocha huyo siku ya Jumapili, kocha mkuu Zoran Maki ndiye alikuwa na jukumu la kuongoza mazoezi ya viungo.

Kikosi cha Simba kinatarajiwa kurejea nchini Agosti 5, mwaka huu kwa ajili ya tamasha la siku ya Simba, huku mchezo wao wa Kwanza wa kimashindano ukiwa dhidi ya Yanga Agosti 13, mwaka huu.

Meneja wa habari na mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema: “Kama ambavyo tuliwatangazia kupitia mitandao yetu ya kijamii siku ya Julai 16, mwaka huu kuhusiana na kocha wetu mpya msaidizi na mtaalamu wa mazoezi ya viungo Karim ambaye mara baada ya kukamilisha taratibu zote rasmi alijiunga nasi Jumapili.

“Mara moja baada ya kuanza kazi kocha ameanza na programu ya ‘Gym’ ambayo inafanyika kila siku mara mbili asubuhi na jioni mara baada ya kukamilisha mazoezi ya uwanjani, hii yote ni katika kuhakikisha wachezaji wote wanakuwa fiti kwa ajili ya msimu ujao hususani mchezo wa Ngao ya Jamii ambao utakuwa wa kwanza wa kimashindano.”


BASHIRI HAPA

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa