Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu amewapongeza Yanga kwa kutinga hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho barani Afrika.
Yanga walitinga katika hatua hiyo jana jumatano wakiwa nchini Tunisia baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya Club Africain.
Kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar Yanga walilazimishwa suluhu ya bila kufungana.
Bao pekee la ushindi kwa Yanga lilifungwa na Stephane Aziz Ki raia wa Burkina Faso dakika ya 78 ya mchezo huo.
Samia ameandika kuwa “Kongole Yanga kwa ushindi na kufanikiwa kusonga mbele katika michuano ya soka la wanaume kwenye kombe la Shirikisho Afrika, msimu wa 2022/23. Nawatakia kila la kheri katika hatua inayofuata.”