Simba Wafunguka Mustakabali wa Matola

Uongozi wa Klabu ya Simba umesema kuwa hawatakuwa na kocha Suleiman Matola kwa muda wa mwaka mmoja kwa kuwa anakwenda kusoma na baada ya kumaliza masomo yake ndipo viongozi watajua kama ataendelea kuwepo kundini au itakuwa tofauti.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally ambaye alidai kuwa Matola ni Simba tangu zamani na anachokwenda kufanya ni kwa faida yake mwenyewe pamoja na klabu hiyo.

Akizungumzia juu ya mustakabali wa Matola ndani ya Simba, Ahmed alisema: “Ni ngumu kutoa majibu ya moja kwa moja kwa sasa kusema kuwa baada ya mwaka mmoja, Matola atakuwa na nafasi hii ndani ya Simba.

“Lakini kila mmoja anafahamu kuwa Matola ni mnyama wa kugalagaza kabisa, anakwenda kusoma kwa faida yake na klabu yetu. Ndiyo maana tukawa tumempa baraka zote alipokuja kuaga.

“Tunaomba amalize masomo yake salama na aweze kufanya vizuri pia. Mengine tutayajua hapo baadae.”

Matola anakwenda kufanya kozi ya ukocha ya leseni A ya Caf. Ambayo itadumu kwa muda wa mwaka mmoja na baada ya hapo atakuwa na nafasi ya kusimama kama kocha mkuu kwenye timu yeyote ile.

Acha ujumbe