UONGOZI wa klabu ya Simba umewaomba radhi mashabiki na wadau wa timu hiyo kwa kushindwa kutimiza ahadi ya kutangaza nyota wao mpya ambaye alipaswa kutangazwa juzi Jumatano, ambapo wameweka wazi sababu za kushindikana kwa utambulisho huo.

Uongozi wa Simba kupitia kwa Meneja wa habari na mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally waliweka wazi kuwa juzi Jumatano walitarajia kumtangaza nyota mpya, ambaye amekamilisha usajili wake kwa ajili ya msimu ujao wa 2022/23 kabla ya kushindwa kukamilisha tukio hilo.

Simba wameweka wazi kuwa kuelekea usajili wao wa mastaa wapya wamebakisha mastaa watatu wapya ambao wanatarajiwa kutangazwa muda wowote, huku taarifa za ndani zikieleza kuwa mastaa hao waliomalizana na Simba ni straika Cesar Manzoki na winga Nelson Okwa kutoka Rivers United ya Nigeria.

Ahmed Ally alisema: “Ni kweli tulikuwa na mpango wa kumtambulisha nyota wetu mpya juzi Jumatano, lakini jambo hilo lilishindikana kutokana na sababu ambazo ziko nje ya uwezo wetu kwa kuwa bado alikuwa hajaripoti kambini Misri.

“Lakini mashabiki wetu hawapaswi kuwa na wasiwasi kwa kuwa tayari maandalizi yote ya kuwatangaza wachezaji waliosalia yamekamilika na tutawatangaza rasmi mara watakaporipoti.”

JIBU

Tafadhali andika maoni yako
Tafadhali andika jina lako hapa