KLABU ya Simba ilikuwa kwenye hati hati ya kukabiliwa na adhabu kutokana na utovu wa nidhamu kwenye mchezo wao dhidi ya Yanga uliopigwa jana kwenye dimba la Benjamin Mkapa na matokeo kuwa sare ya 1-1.
Kwa taarifa iliyotufika hii leo kwenye dawati letu la habari ni kwamba Simba haitaadhibiwa na Bodi ya Ligi kwa wachezaji wake kuonyeshwa kadi tano za njano kwenye Dabi ya Kariakoo iliyochezwa Jumapili Oktoba 23, 2022.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Sheria, Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura. Amesema kuwa “adhabu itatolewa iwapo timu itapata zaidi ya kadi tano za njano.”
Katika mchezo huo ulizishudia timu zote zikishambuliana kwa kasi sana na kila timu ilitengeneza nafasi za magoli lakini haikuwa hivyo, kitu ambacho kiliwatoa wachezaji mchezoni na kujikuta wakifanya madhambi na kuadhibiwa kwa kadi za njano.
Mchezo wote kwa ujumla ulikuwa na kadi za njano tisa (9) huku kwa upande wa Yanga wakiambulia kadi nne (4) pekee na Simba wakipata kadi za njano tano (5), hivyo wengi walikuwa na wasiwasi kuwa klabu hiyo ya Msimbazi itaadhibiwa kutokana na kosa hilo.
Kwa mujibu wa takwimu za mechi 11 zilizowakutanisha watani wa jadi kwenye Ligi Kuu ikiwemo ya jana, Yanga ameshinda mechi 2, na Simba ameshinda Mechi 2, sare zikiwa ni 7.