Nyota wa zamani wa NIGERIA mkongwe Taribo West amelaumu vitendo vya ngono kwa wachezaji wenzie kwenye hoteli ilikuwa sababu ya kutupwa nje ya Kombe la Dunia la 1998 dhidi ya Denmark. Super Eagles ilikuwa moja ya timu bora za mashindano ya World Cup huko Ufaransa baada ya kufanya vyema katika hatua ya makundi wakimaliza juu ya kundi kwa alama sita mbele ya Uhispania, Bulgaria na Paraguay. Lakini tofauti na matarajio ya wengi katika hatua ya 16 Nigeria ikatupwa nje na Denmark kwa kipigo kizito cha mabao 4-1.
Beki huyo wa zamani wa Inter na AC Milan Taribo West amefunguka kuwa umaarufu na kujiamini kulikopitiliza kwa wachezaji wa Nigeria ndio lilikuwa anguko la Nigeria kwenye WorldCup. West ambaye kwasasa ana umri wa miaka 46 alidai wachezaji wenzake walichoka kwa kulala na mashabiki (wanawake) usiku kabla ya Mchezo wao wa hatua ya 16 dhidi ya Denmark.

Aliliambia Jarida la Nigeria la The Punch: “Wanawake walikuwa Waafrika ambao walikuja kutazama mashindano hayo na waliipenda timu yetu kwa sababu ya jinsi tulicheza kwenye hatua ya makundi. Kwa hivyo, ilikuwa rahisi kwa wachezaji hawa kuwaingiza kwenye vyumba vyao. “Pia ninachojua ni kwamba wachezaji wengine walifungia wanawake kambini, nimeona hiyo. Ndio maana siku ya mechi, unaweza kuona wachezaji wengi hawakuwa na nguvu ya kupambana na wachezaji wa Denmark.”

Kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia dhidi ya Denmark 1998
“Walikuwa wamechoka baada ya kujishughulisha zaidi na usiku uliopita na wanawake. Nilichukizwa sana na nilikuwa nikiwapigia kelele uwanjani, nilikasirika sana. Walifanya haya yote kwa sababu walidhani tutaipiga Denmark.”
Nigeria ya ’98 ilijumuisha nyota wa ulimwenguni kama Jay Jay Okocha na mshambuliaji wa zamani wa Arsenal, Nwankwo Kanu. Licha ya kupewa nafasi kubwa ya kushinda dhidi ya Denmark, Super Eagles iliondoshwa kwenye hatua ya 16 na tangu hapo haijawahi kwenda zaidi ya hatua hiyo kwenye mashindano ya Kombe la Dunia.

