Janga la virusi vya Korona, kitaalamu likifahamika kama Covid19 limekwamisha shughuli nyingi za kiuchumi na kijamii. Limegusa wadau wengi mno ulimwenguni kwote huku mamia ya watu wakipoteza maisha hasa barani la Ulaya, huku Italia wakiwa wanaongoza kwa idadi ya vifo.
Sekta ya michezo pia imeathirika kwa kiasi kikubwa wakati ligi kubwa zikilazimika kusimama, ikiwa ni jitihada za kuzuia maambukizi, hasa kipindi hiki watu wakiwa wanashauriwa kukaa karantini na kuchukua tahadhari zingine za kitaalamu.
Kutokana na athari ya virusi hivi ulimwenguni kwote, baadhi ya mastaa na wadau wakubwa wa michezo wameamua kutoa mchango wao dhidi ya kupambana na virusi hii.
Baadhi ya wadau wakubwa wa soka waliotoa mchango wao ni Ronaldo (CR7) na wakala wake Jorge Mendes, Lionel Messi, Pep Guardiola, Mourindho, ikiwa ni baadhi yao tu.
Messi ametajwa na jarida la Marca kuwa ametoa mchango wake ambao utagawanywa katika Hospitali kadhaa za jiji la Barcelona na kituo kingine cha Afya kilichopo nchini kwake.
Meneja wa Manchester City, ambaye pia amewahi kuwa mchezaji na meneja wa Barcelona naye alitoa mchango wake katika kampeni iliyoanzishwa na chuo kimoja cha kitabibu jijini Barcelona kwa kushirikiana na taasisi ya Angel Soler Daniel.
Staa wa Juventus Cristiano Ronaldo na wakala wake Jorge Mendes wanashirikiana kusaidia vituo vitatu vinavyowahudumia waathirika wa virusi corona pale Ureno. Vyanzo vya habari vinataja kuwa wawili hawa wanachangia zaidi ya paundi milioni 1 kwa vituo hivyo vitatu.
Michango ya wadau hawa wote kwa pamoja imegusa huduma za waathirika, dawa, vifaa vya matibabu na kupumulia pamoja na vitanda.
Wadau wa michezo pamoja na watu wote ulimwenguni wanaunga mkono jitihada za kupunguza ueneaji na kutokomeza kabisa janga hili. Shirika la Afya Duniani (WHO), Benki ya Dunia (WB) na wadau wengine kwa pamoja wanafanya jitihada kuhakikisha chanjo inapatikana haraka kadri inavyowezekana ili shughuli zote, ikiwepo michezo na shughuli zingine za kijamii na kiuchumi kuendekea.

