Yanga Jumamosi katika kilele cha wiki ya Mwananchi walikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Vipers ya Uganda, mchezo ambao ulipigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mara baada ya kipigo hicho cha Jumamosi, Yanga sasa wanajiandaa na mchezo wa ufunguzi wa Ngao ya Jamii ambapo watakuwa wenyeji wa Simba katika mchezo huo ambao unatarajiwa kupigwa Agosti 13, mwaka huu.
Kocha Nabi alisema: “Kwetu mchezo wa Jumamosi ulikuwa kipimo kizuri kuelekea mchezo dhidi ya Simba, nafahamu kuwa mashabiki wengi wa Yanga walitamani kuona tunashinda Jumamosi kwa kuwa ilikuwa siku muhimu kwao, lakini kiuhalisia kwetu matokeo ya mchezo ule hayakuwa na umuhimu sana, bali kuangalia maendeleo ya kikosi.
“Tumeona ni kipi ambacho wachezaji wetu wamekipokea katika siku takribani kumi za kwanza ambazo tulikuwa kambini, tumetoa programu maalum kwa wachezaji wote ili kufanyia kazi mapungufu yote ambayo tuliyaonyesha na naamini tutakuja tukiwa tofauti sana siku ya Jumamosi kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu.”

