Kwa mujibu wa Waziri wa Michezo wa Ufaransa, michezo ya mbio za baiskeli za wanaume Tour de France ambazo hufanyika kila mwaka zinatazamiwa kufanyika bila kuwepo na mashabiki.
Kutokana na mlipuko wa Virusi vya Korona (Covid19) michezo mingi ulimwenguni imesitishwa na kutarajiwa kufanyika baadaye pale hali itakaporejea kuwa sawa. Nguvu zote zimeelekezwa kupambana na janga hili kwa sasa.
Wakati michuano ya michezo mbalimbali mikubwa ulimwenguni kama Euro 2020 na Michezo ya Olympic kule Tokyo ikiwa imeahirishwa, Tour de France bado inatarajiwa kuwepo mwezi Juni japokuwa kutakuwa na mabadiliko kadhaa kulingana na hali halisi itakapokuwepo wakati huo, na kuna uwezekano pia wa kuahirishwa.

Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Michezo ya Ufaransa, kama ilivyoripotiwa na jarida la Reuters Alhamisi, wizara inaona bado ni mapema mno kufanya maamuzi magumu kama michuano hiyo ya mbio za baiskeli maarufu kama Tour de France iahilishwe kutokana na janga hili la Covid19.
Wizara imeweka wazi kuwa kuna mda wa kufanya kila kitu na kwa sasa jitihada zimeelekezwa kwenye pambano hili la dharura. Hivyo kuna haja ya kuelekeza jitihada kwa pamoja kuupanda mlima uliopo mbele kisha mambo mengine yatafikirika hapo mbeleni.
Hata hivyo, kwa mujibu wa kituo kimoja cha redio cha ndani ya Ufaransa kilinukuu taarifa ya wizara hiyo kuwa inafikiria michuano hii kufanyika bila mashabiki ili kupunguza hatari ya maambukizi.

