Sadio Mane Mshambuliaji wa Bayern Munich usiku wa jana ameshika nafasi ya pili katika tuzo za mwaka huu za Ballon d’Or, nyuma ya Kareem Benzema aliyefanikiwa kutwaa tuzo hiyo ya mchezaji bora wa dunia.
Japo hakutwaa tuzo ya Ballon d’Or, Mane, raia wa Senegal amefanikiwa kutwaa tuzo ya kwanza ya Socrates Award, kwa mchezaji aliyejitoa kusaidia kutatua changamoto za kijamii.
Ni tuzo ya kwanza kutolewa ikilenga kuhamasisha wachezaji kushiriki kusaidia jamii zao.
Benzema bora Uwanjani, Mane bora mtaani
Miezi 3 kabla ya kutolewa kwa tuzo za Ballon d’Or mwaka huu, kila mmoja anayefuatilia soka alijua nani atatwaa tuzo hiyo. Kareem Benzema alikuwa na msimu mzuri zaidi katika maisha yake ya soka
Aliisaidia klabu yake ya Real Madrid kutwaa taji la klabu bingwa Ulaya pamoja na ligi ya Hispania (Laliga), akifunga mabao 44.
Ni tuzo isiyo na mashaka kabisa, kutokana na mchango wake mkubwa kwa klabu na timu yake ya taifa ya Ufaransa.
Mpaka leo Benzema amefunga katika michezo 62 ya ligi ya mabingwa Ulaya, mabao yaliyosaidia timu yake kupata ushindi mechi 45, sare 11 na kupoteza michezo 6 tu. Ana mabao 86 katika ligi hiyo, yanayomfanya kushika nafasi ya 4 kwa wachezaji wenye mabao mengi ya michuano hiyo. Nyuma ya Cristiano Ronaldo (140), Lionel Messi (127) na Robert Lewandowski (91).
Sadio Mane hana takwimu za kutisha katika michuano hiyo, lakini na yeye amekuwa msimu wa kuburisha. Aliisaidia Senegal kutwaa ubingwa wa Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza, akifunga mabao muhimu na kuingoza pia kufuzu kombe la dunia litakaloanza Qatar mwezi ujao.
Alitwaa FA Cup na kombe la ligi akiwa na Liverpool na kuisaidia klabu hiyo kucheza fainali ya ligi ya mabingwa Ulaya, walipopoteza dhidi ya Real Madrid.

Hakuna ubishi Mane ni mchezaji bora wa Afrika, mchezaji bora wa pili wa dunia, lakiniuzuri wake unaonekana ndani ya uwanja na mtaani, nje ya uwanja.
Sifa ya Mane mtaani Afrika ni kubwa, ni ya kutukuka, hakuna asiyejua anachokifanya nyumbani kwa Senegal, hatua iliyompa tuzo muhimu ya kwanza kwa mtu aliyeisaidia jamii.
Mwisho wa Twitter ujumbe
Atasalia kuwa mchezaji bora wa mioyo ya watu daima
Kuna Mane wakati aliwahi kunukuliwa “Kwa nini nihitaji magari 10 ya Ferraris, saa 20 za almasi, au ndege mbili? vitu hivi vitanisaidia nini mie na dunia? Nilikwa na njaa, nahitaji kupambana uwanjani; nilipitia nyakati ngumu, kucheza mpira bila viatu, sikusoma, na mambo mengine, lakini leo kile ninachokipata kwa sababu ya soka, naweza kusaidia watu,”.
Hilo linajionyesha kwa anachokifanya kwa jamii. Amefanya mambo mengi lakini yale yanayofahamika ni pamoja na;

Amejenga hospitali, msikiti, na uwanja wa mazoezi, na kuchangia kiasi cha £250,000 kujenga shule na kugawa laptop.
Alichangia £41,000 kusaidia mapambano dhidi ya Corona nchini Senegal
Aliidhamini moja ya hospital nchini humo kwa gharama ya £455,000
Ametengeneza kituo cha mafuta kijijini na sasa anatengeneza ofisi ya posta, achinilia mbali huduma za internet.
Huyu ndio Sadio Mane, ambaye aliwahi kusafisha vyoo vya msikiti kwenye uwanja wa King Power masaa machache baada ya ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya Leicester.
Benzema amekuwa akisaidia pia jamii kwa nafasi yake, lakini alichokifanya kwa jamii yake Senegal na maeneo mengine linamtofautisha na wengi.
Sadio Mane maisha ya maelfu ya watu na kuboresha maisha ya jamii yake. Na haya ndiyo yatakayomfanya abakie miiyoni mwa watu kwa miaka mingi, pengine hata nafasi yake kwenye tuzo ya Ballon d’Or.
Unaweza kutazama video za uchambuzi wa michezo na matukio kwa kugusa Video Hii