KIUNGO wa Yanga, Gael Bigirimana, ameanza na mkwara mzito kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba kwa kuwaambia wapinzani wao kwamba, wanapaswa kujipanga vizuri.
Bigirimana aliyewahi kucheza Ligi Kuu ya England akiwa na Newcastle United, amejiunga na Yanga kwa mkataba wa mwaka mmoja akitokea Glentoran ya Ireland Kaskazini.

Bigirimana amesema kuwa: “Binafsi kwangu utakuwa ni mchezo muhimu kwa sababu ni dabi ambayo imekuwa ikifuatiliwa na watu wengi Afrika Mashariki na Kati.
“Kwa upande wangu nitakachokiangalia ni suala moja la kuhakikisha nakuwa msaada wa timu kupata ushindi.
“Simba ni moja kati ya timu kubwa kama ilivyo Yanga, lakini jambo la msingi kwetu ni kuwaheshimu kama watani, lakini suala la kupata matokeo ni kipaumbele chetu cha kwanza kwa kuhakikisha rekodi ya msimu uliopita tunaiendeleza.”

